MAELEZO YA PASIPOTI MPYA ZA KI-ELEKTRONIKIA, TANZANIA

Idara ya Uhamiaji Tanzania  imeanza kutoa pasipoti mpya za Kieletroniki tangu tarehe 31/1/2018.Ubalozi unawashauri kuomba pasipoti mpya mkiwa nyumbani likizo na kuomba kitambulisho cha taifa kitakachowawezesha mambo mengi.

MAOMBI YA PASI ZA ZAMANI UBALOZINI YAMESITISHWA

Ubalozi umepokea barua kutoka Idara ya Uhamiaji ikiarifu kuwa kuanzia tarehe 30 Aprili 2019 maombi ya pasipoti za zamani – Machine Readable Passports (MRP) yamesitishwa kupokelewa kutoka kwa Watanzania waishio nje (Diaspora). Ubalozi pia unapenda kuwakumbusha kuwa mwisho wa matumizi ya pasipoti za zamani za MRP ni tarehe 30 Januari 2020.

Ubalozi wa Tanzania Sweden haujafahamishwa tarehe kamili ya kufungiwa mitambo hiyo ingawaje kwa mujibu wa maelezo ya Uhamiaji ni kwamba Ubalozi wetu utafungiwa hivi karibuni.

Ubalozi unapenda kuwashauri wale watakaobahatika kwenda nchini Tanzania watumie muda huo wa likizo kuombea nchini pasipoti hiyo mpya. Waombee nyumbani kwa kujaza maombi ya pasipoti za Kielektroniki (e-passport) na kufuata taratibu za mwombaji wa pasi akiwa nyumbani.

Kwa wale wenye dharura kuhusu vibali vya kuishi katika nchi walizopo na hawawezi kusafiri kwenda Tanzania kupata pasipoti, wawasiliane na Ubalozi kwa mashauriano zaidi.

Poleni sana kwa usumbufu utakaojitokeza lakini tunashukuru sana kwa ushirikiano wenu. Tutaendelea kupeana taarifa kupitia Tovuti hii pindi tutakapofungiwa mitambo husika hapa Stockholm.