TAARIFA KWA WATANZANIA
TAARIFA IIUbalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Berlin Ujerumani, pamoja na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Stockholm Uswidi, tunapenda kuwataarifu watanzania wote wanaotokea Ukraini kuelekea katika mipaka ya magharibi ya nchi hiyo kama ifuatavyo:
(1) Tunaendelea kuratibu kwa karibu taarifa za Watanzania wanaotoka Ukraini kuelekea nchi za Poland, Slovakia, Hangari na Romania.
(2) Tunatambua na kutoa shukurani kwa mchango mkubwa wa jumuiya za Watanzania (diaspora) ambao wamekuwa wakishirikaina nasi kwa karibu kuwasaidia Watanzania wanaovuka mpaka kutokea Ukraini kuingia katika nchi za Poland, Slovakia, Hangari na Romania.
(3) Baada ya kubainisha maeneo ambayo idadi kubwa ya Watanzania wanaelekea wakitokea Ukraini, na kwa kuzingatia hali halisi iliyoko mipakani, mifumo ya usafiri na uzoefu katika masaa 48 yaliyopita, tunapeleka Maafisa Ubalozi katika miji ya Przemyśl (Poland) na Budapest (Hangari).
(4) Watanzania wanaotokea Ukraini kuelekea Poland wawasiliane na Afisa Ubalozi kupitia nambari ya simu +46720494576; na wale wanaoelekea Hangari wawasiliane na Afisa Ubalozi kupitia nambari ya simu +4915215117558 kwa uratibu. Nambari zote zinapatikana katika mtandao
wa WhatsApp.
(5) Ikiwa hali halisi italazimu baadhi ya Watanzania kuelekea katika maeneo mengine zaidi ya haya yaliyopendekezwa, inashauriwa wawasiliane na maafisa Balozi kupitia nambari za simu zilizoainishwa katika taarifa hii
(6) Licha ya mazingira magumu yanayowakabili, tunawasihi Watanzania wote wanaokimbia mapigano nchini Ukraini, na wale ambao bado wamekwama katika maeneo yenye mapigano kuwa watulivu ili kulinda usalama wao, huku juhudi mbalimbali zikiendelea kufanyika kwa kuwasiliana na mataifa na mashirika mbalimbali ili kuwaondoa katika maeneo yenye hatari.
(7) Tunatoa shukurani kwa kampuni ya Global Education Link pamoja na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa Watanzania walioko Ukraini ambao wamekuwa wakishirikiana nasi kwa karibu katika kipindi hiki kigumu.
Tunaendelea kushukuru kwa ushirikiano tunaoupata, na tutaendelea kutoa taarifa au maelekezo mara kwa mara.